Monday, 17 December 2012

KOFFI KUTOA BURUDANI DAR ES SALAAM



MSANII Antoine Agbepa Mumba almaarufu kama Koffi  Olomide (56) ambaye  ni mahiri  katika uimbaji wa miondoko ya Soukous  yupo nchini kutoa burudani  Jumamosi  Desemba 15 2012.
Ni msanii mwenye majina mengi yaliyompa umaarufu kama Grand Mopao, Mokonzi, Tcha Tcho king, atatumbuiza  na bendi yake  ya Quartin Latin  katika uwanja wa Leaders Club Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 Akiwa nchini kwa  uratibu wa Kampuni ya Prime Time Promotions Olomide ametua na muimbaji nyota wa bendi hiyo Sindy ambapo watapamba miaka 13 ya kuanzishwa kwa Kampuni ya Clouds FM.
Mbali ya bendi ya Koffi pia bendi pinzani nchini FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ wakiwa chini ya uongozi wa Kyala Matala ‘Nyoshi El Saadat’ watatoa burudani sanjari na bendi ya The African Stars Entertainment ‘Twanga Pepeta’ nao wamesema kwamba wamejipanga kwa kutoa burudani kesho.
Akizungumza jana Kiongozi wa Twanga Luiza Mbutu anasema kwamba watatumia onesho hilo kwa kujifunza muziki kutoka kwa Koffi kwani kundi hilo linaongozwa  nha nguli wa muziki duniani.

Aidha katika hali nyingine haijawahi kutokea kwa bendi mbili pinzani za Twanga na FM Academia kupanda katika jukwaa moja na onesho moja  hivyo  siku ya kesho itakuwa ni siku maalumu kwa wapenda muziki kupata burudani kutoka kwa bendi mbili kubwa nchini na moja ya kimataifa.
Bendi nyingine itakayosindikiza katika onesho hilo ni Skylight  iliyozinduliwa mwaka huu.Kiingilio ni sh.10,000 kabla na sh. 15,000 mlangoni.
Alikotoka
Koffi  Ambaye ni mwanamuziki mahiri msomi pia mtunzi mzuri wa nyimbo  amabye alianza kuonesha umahiri wake kati ya mika 1970 na 1980 ambako alikua akimuandikia nguli wa muziki nchini Janhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Papa Wemba enzi hizo akiwa na bendi ya  Orch Viva La Musica.

Wakongomani wengi wanamkubali  Koffi Olomide kuwa yeye ni chuo cha mafunzo kwa wanamuziki wengi wa DRC, mmoja wa wanao ukubali ujabali wa muziki wa Olomide ni pamoja na mwanamuziki wa kikongo anayeishi jijini Nairobi nchini Kenya Kasongo wa Kanema  anayetumikia katika bendi ya Super Mazembe hukuakisema “Koffi ni msafi katika muziki na tungo zake pia kwani ujumbe anaoutoa unakuwa wenye uzito na maana kubwa”.
“Nyimbo nyingi za Olomide ziko kipekee na ikipigwa tu utatambua kuwa sasa mopao yuko hewani,kutokana na ujuzi wa aina yake  mpangilio murua  ndio unaompatia mrehjesho mzuri, kuuza vema kazi zake na kumpatia umarufu”anasema Kanema.
Kasongo anasema kwamba kupendwa kwa muziki wa Koffie sio kwamba kumekuja bure amesoma , amejituma na huumiza kichwa kila anapotaka kuachia albamu hio ndiyo siri kubwa ya muziki wa Koffie.
Kwa wadau wa muziki watakumbuka moja ya kibao kilichotamba kuwa ni 'Papa Plus', 'Futa Djalon', 'Andraa', 'Loi', 'Mbirime', 'Micko', 'Attentat' na 'Ngounda'.
 Pia Koffi amewahi kurekodi na mwanamuziki Nyboma Mwanindo wimbo wa 'Anicet' na 'Papa Bonheur'
Changamoto  katika muziki
Kwa muda wa miaka mitatu iliyopita mwanamuziki huyu  hakuweza kufanya maonesho barani Ulaya kutokana nakukabiliwa na kesi ya kunyanyasa wacheza shoo wake huku wakihusishwa na masula ya kisiasa anti-Kabila.
Koffi aliwekwa chini ya ulinzi Agosti 15, jijini Kinshasa, pia alitetewa na jopo la mawakili wapatao 10.
Kama ilivyo kawaida ya wanamuziki siku zote kusaka maslahi yao ,mwaka 1998 Koffi alionja chungu  ya muziki baada ya onesho kubwa lililofanyika kwenye ukumbi wa Olympia  jijini Paris bendi yake ilivunjika.
Ilivunjwa na baadhi ya wanachama na wanamuziki walioenda kuanzisha  bendi ya Orchestre Quartier Latin Academia.
Historia yake kwa ufupi
Alizaliwa Julai13, 1956, Kisangani kabla familia yake haijahamia Kinshasa DRC huku mama yake akiwa mwenye asili ya huko na baba yake ni mwenye asili ya kutoka nchini Sierra Leone.
Ametoka katika familia yenye maisha na uwezo wa kati  
Mwaka 1970  akitokea nchini Ufaransa alijiunga na  bendi ya Viva la Musica  iliyokuwa ikimilikiwa na  Papa Wemba ambapo alikuwa katika nafasi za ‘ music composer’ na mwandishi wa nyimbo na baadaye akaja kuwa mwimbaji mahiri.
Mwaka 1986, alilipa kisogo kundi la Viva la Musica  na kuanzisha  bendi yake ya Quartier Latin,ambayo ilikuwa imesheni  ala zote za muziki, waimbaji,  na wacheza shoo huku kundi zima likiwa na wanamuziki wapatao 30.
Kuanzia hapo Koffi ndipo alipokunjua makucha yake na kujijengea jina Afrika Mashariki, Kati, Kusini na Afrika Magharibi akitamba na Tcha Tcho mtindo wa soukous.
Mwaka 2002 alipata tuzo ya muziki ya Kora Award  akiwa kama mwanamuziki bora Barani Afrika.
Mafanikio
Wanamuziki wengi wenye asili kutoka nchini  DRC wengi wamepita katika mikono yake  kama vile Fally Ipupa, ambaye Koffi alimpika kwa muda wa miaka 10  ndani ya bendi yake ya Quartier Latin , kabla mwanamuziki huyo hajaamua kua solo na hatimaye kuanzisha bendi yake.
Kwa sasa  Fally  ni kati ya  mwanamuziki wenye heshima na jina kubwa duniani ambaye anafanya kazi na kuisshi nchini Marekani huku akifanya kazi kwa karibu na G-Unit of 50 Cent’s Olivia.
Nyota mwingine katika muziki aliyepitia katikia mikono ya Koffi ni Ferre Gola, baada ya kuachana na kundi la Werra Son Wenge Musica Maison Mere.
Kama hiyo haitoshi  tunda lingine adhimu la kazi ya Koffi ni Montana Kamenga ambaye baada ya kujiona amewiva kimuzi kutoka kwa Koffi alikimbilia kwa General Defao Matumona.

Pia wengine waliopikwa na Koffi ni  Fele Mudogo, Sam Tshintu, Suzuki 4x4, Buro Mpela na Soleil Wanga.
Kutokana na umahiri wake katika muziki Koffi amewahi kushirikishwa katika  miradi mbalimbali ya muziki ikiwa ni pamoja na ‘Salsa music project’, ‘Africando music project’.
Albamu:
Effrakata, Tcha Tcho, Magie, Haute De Gamme- Koweit, Rive Gauche, Pas de Faux Pas, Live A Bercy, Attentant, Ngounda, Le Rambo du Zaire, Golden Star,  Noblesse Oblige, V12, Ultimutum, Loimore, Monde Arabic na Abracadabra inayotamba hivi sasa.
Makala imeandaliwa na Khadija Kalili na Msaada wa Mashirika. 


No comments:

Post a Comment