Wednesday, 12 December 2012

MIAKA 20 YA CLUB BILICANAS YAFANA


Na Khadija Kalili

ILIKUWA ni siku ya aina yake ambapo licha ya kuwa na hali ya hewa ya mvua iliyonyesha na kusababisha muziki wa bendi ya Skylight iliyokuwa ikitoa burudani nje ya ukumbi wa Club hiyo lakini mashabiki bado waliendelea kuingia  na kujumuika kwenye sikukuu hiyo.

Mbali na mvua mashabiki hao ambao walijumuika katika maadhimisho hayo ambayo yamefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 13 ya kuanzishwa kwa Kampuni ya Clouds FM.

Usiku wa Jumamosi Desemba mosi  utabaki kuwa ni siku ya kumbukumbu maalumu ya kutimiza miaka 20 ya Club Bilicanas ambayo pasina shaka ni Club inayotajwa kuwa ni yenye hadhi ya Kimataifa Barani Afrika na hata Ulaya.

Katika sherehe hiyo ambayo keki ilikatwa na mfanyakazi aliyedumu kwa kipindi chote hicho kwenye Club hiyo ambaye ni Monica almaarufu kama Da Monica huku wengine wakimwita Mamdogo alikata na kumlisha Mkurugenzi wa Kampuni ya Bilicanas Group Dk. Lilian Mtei Mbowe.

Mbali ya tukio la kukata keki na kumlishana  Mkurugenzi pia wadau mbalimbali waliohudhuria tukio hilo nao pia walipata fursa ya kula kipande hicho cha keki .

Akizungumza na Tanzania Daima nje ya ukumbi huo  mmoja wa Wakurugenzi wa Clouds  FM Ruge mutahaba anasema kwamba ni jambo la kumshukuru mungu kwani kwa Kampuni zote hapo zilipofikia zimepitia changamoto nyingi na siyo jambo rahisi.

Kuanzisha Kampuni na hasa katika masula ya burudani siyo kazi rahisi hata kidogo jambo kubwa ni namna ya kuiendeleza ndiyo kazi kubwa.
 
Kadhalika baadhi ya wadau mbalimbali wa tasnia ya burudani nchini ambao waliweza kufanya mahojino na Tanzania Daima wanasema kwamba wanatoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Club Bilicanas kwani tangu kuanzishwa kwake miaka 20 imeweza kufungua milango ya kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka anasema kwamba yeye binafsi anakumbuka namna Club Bilicanas ilivyoweza kujizolea umaarufu tangu ilipoasisiwa huku na yeye akiwa ni kati ya wadau na mashabiki wakubwa wa Club hiyo.

“Nakumbuka namna Club Bilicanas ilivyokuwa ikitoa raha kwa mashabiki wa hapa Jijini Dar es Salaam na hata  nje ya jiji na kuweza kuvuka mipaka hadi nje ya nchi” anasema Asha.

Binafsi nina kila sababu  ya kuishukuru Club Bilicanas kawani  ndani ya miaka 20 tumekuwa tukifanya kazi kila siku ya Jumatano katika usiku wa Mwafrika ‘Africa Nite’ hivyo kuweza kugawana riziki kwa namna moja ama nyingine.

Asha anasema katika miaka ya nyuma  Club Bilicanas iliweza kuvumbua vipaji vya kundi la kunengua la Bilibums ambalo liliwavumbua  wanenguaji mahiri ambao ni Hassan Mussa ‘Super Nyamwela’ ambapo pia alikuwepo aliyekua mnenguaji mahiri Aisha Mbegu ‘Queen Aisha  aliyeitumikia kwa miaka kadhaa bendi ya Twanga Pepeta .

Kwa sasa wote baada ya kung’ara na kundi hilo waliweza kuchukuliwa katika  bendi mbalimbali ikiwemo Twanga Pepeta na nyinginezo.


Historia inaonesha kwamba bendi mbalimbali ikiwemo makundi kadhaa yaliwahi kupamba onesho la usiku wa mwafrika , usiku ambao umekuwa kivutio kikubwa zaidi ndani ya Club hio .

Baadhi ya bendi zilizowahi kunogesha usiku huo ni pamoja na bendi ya The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’ ambao wanapiga muziki wao katika mtindo wa mduara.

Shamrashamra za kuadhimisha miaka 20 ya Bilicanas  zitaendelea  kwa muda wa mwaka mmoja hadi mwanzoni mwa mwezi Januari ifikapo mwakani.

Jumapili Desemba 2, ndani ya Club Bilicanas wazanii nyota wa muziki  wa kizazi kipya walitoa burudani ambao ni Ommy Dimpoz, Linah, Recho, Amini, Richie Mavoko, Barnaba, Makomandoo, Rais wa Masharobaro Bob Junior na nyingine mbalimbali.

No comments:

Post a Comment